Je! Beef hii ni Dar dhidi ya Arusha?




“These rap cats softer than a new born baby bottom... Eti big fish in this ocean... My pussy cat eats that shit..” Ni maneno yanayosemeka katika ukuta (wall) wa Harry Kaale maarufu kwa jina la One The Incredible aka Moko wa Miujiza. Ni fataki alilolielekeza kwa Joh Makini kuashiria kuwa vita katika ya Weusi kundi huru linalojumuisha rappers kutoka Arusha ambao ni yeye mwenyewe Joh, nduguye Nikki wa Pili, Gnako, Bonta aka Maarifa, Lord Eyez na wengine dhidi ya Nikki Mbishi aka Baba Malcom na One the Incredible na washirika wengine wa Lunduno na Illmatic imeiva.     
     
Chanzo cha ugomvi huu wa kimuziki kati ya pande hizi mbili unaaminika kuanza katika kipindi cha mwaka mmoja na kitu uliopita.  Katika mazingira mengi ya kuzuka kwa beef za hiphop mashabiki huwa na asilimia nyingi za kwao zinazopelekea wasanii fulani kupaniana kiushindani hali inayosababisha beef ya kawaida ama kali. Jina la “Nikki”ni sehemu moja wapo ya kuwepo kwa tension kati ya Nikki wa Pili na Nikki Mbishi. Watu walianza kumsikia kwa ukamilifu Nikki wa pili katika wimbo alioimba na ndugu yake Joe Makini “Niaje ni Vipi” . Hapo ndipo mashabiki wa hiphop Bongo wakatambua kuongezeka rasmi kwa orodha ya wasanii wenye uwezo mzuri kiuandishi nchini wanaotokea Arusha. Baadaye Nikki wa Pili alisimama mwenyewe kwenye ngoma aliyomshirikisha Rama D “Good Boy”.
Kwa upande wa Nikki Mbishi, safari yake ya kuwa nyota katika hiphop ilikuwa tofauti kidogo. Yeye alianza kujulikana nchini kabla hata hajaachia wimbo uliorekodiwa na kusambazwa katika mkondo mkuu wa muziki wa Tanzania. Nikki Mbishi alijizolea umaarufu katika kipindi cha Bongo Flava cha Clouds Fm kwa uwezo wake wa kuchana ,mitindo huru (Freestyles). Kwa mujibu wa watu wanaomfahamu kwa ukaribu, wanasema Nikki Mbishi ana uwezo wa kurap kwa freestyle kwa masaa kadhaa bila kurudia mada na ndiye msaani ambaye One anamhofia kuliko wote nchini.

Baada ya kuvikwa taji la mchanaji bora wa mitindo huru enzi hizo, Nikki Mbishi aliongezea msumari mzito kwa mashabiki wake katika wimbo wake wa “Punch za kwenye Line”  Kama jina la wimbo unavyojieleza, wimbo mzima ulijaa uandishi mzito unaohitaji muda mrefu kuchambua na kupata maana halisi ya kila alichokuwa anatema (spit), sifa ambayo imekuwa ikipelekwa pia kwa maswahiba wake One na Stereo. Mashabiki wa wasanii hawa wanaofanana majina ya mwanzo wakawa na shauku ya kujua uwezo wa kila mmoja ili kupata jibu na ni mkali zaidi ya mwenzie. Jibu wanalo mashabiki wenyewe. Lakini hapo ndipo story hii iliyotawala vinywa vya mashabiki wa hiphop nchini, vituo vya radio na mijadala katika mitandao ya kijamii kwa sasa kuhusu beef kati ya Weusi na Nikki Mbishi na One ilipopandikiza mbegu zake.

Kwa mujibu wa story za chini kwa chini ni kwamba Nikki Mbishi alimshirikisha Rama D kwenye chorus ya Punch za Kwenye Line lakini baadaye Rama D akaomba kuondolewa sauti zake kwenye wimbo huo kwakuwa hakutaka kugombana na Joh Makini ambaye inasemekana hakuwa anampenda Nikki Mbishi. Kutokana na uamuzi huo wa Rama D, Duke ambaye ndo producer wa wimbo huo pamoja na uongozi wa MLAB wakaamua kumchukua Grace Matata kufanya chorus. Kwao MLAB huo ulikuwa ni uamuzi uliofanyika kwa kutopenda kwakuwa Grace kipindi hicho alikuwa bado msaani mchanga na asiyejulikana kwa wengi kama ilivyo sasa.

 Baada ya hatua hiyo kukaanza kuzuka maneno kutoka kwenye kambi ya River Camp Soldiers na kuonekana kuwepo uwezekano wa kambi hiyo kuwadiss Lunduno (kundi huru lililopo maskani wanapotokea Stereo na nikki ambao kwa sasa wamejitoa). Kambi ya Lunduno kupitia One ikatupa jiwe lake kuelekeza kwa River Camp soldiers ambao kwa sasa wapo ndani ya kundi kubwa linalowajumuisha pia member wa Nako 2 Nako liitwalo “Weusi”.

Kwa mujibu wa mahojiano na Clouds FM, One alidai kuwa alirekodi wimbo katika studio za Tongwe Records ambayo kuna mstari unasema siwezi kuuza kura yangu kama Bonta akimaanisha wimbo wa Bonta uitwao “Nauza Kura”. Pamoja na dongo hilo lililoekezwa kwa Bonta, hakuna jibu la wazi kutoka kwa Bonta zaidi ya kujibu “Sina tofauti nao” alipoulizwa kuhusu msimamo wake.

Katika mahojiano hayo One alisema anashangaa kujikuta yupo kwenye beef na Weusi wakati anawasiliana mara kwa mara na Joh Makini pamoja na Lord Eyez ambao kwake ni kama kaka zake kimuziki. Japokuwa kauli hii ya One inakinzana na status yake hapo mwanzoni kabisa mwa makala haya ambapo anamdiss wazi wazi Joh Makini.

Mahojiano hayo yalifanyika kutaka kuwepo ufafanuzi kuhusiana na status ya facebook aliyoiweka jumatano (28/03/2012) iliyosema: “Niki wa pili: sijakutaja, usijihusishe, this is none of your biz..Do you homo…”



One alifafanua kuwa sababu ya kuandika status hiyo ni kutokana na hatua ya Nikki wa pili kumtumia ujumbe Nikki Mbishi ambao Mbishi alimfowadia ukisema kuwa wao akina One bado ni wadogo kwenye muziki na hawawezi rap, pia album ya Mbishi inasound kama single moja.

Kuhusu namna anavyowachukulia members wa Weusi, One anasema “Ni wazi kuwa siwakubali Weusi, si kama nawakosea heshima bali ni jibu nitakalokupa kama ukiniuliza kama shabiki, mimi si shabiki wao, Ujue nina waheshimu wao kama kundi lenye mafanikio kulingana na kile wanachofanya, hivyo hiyo ni heshima kubwa niliyonayo kwao lakini mimi si shabiki wao” (phatbeattz.blogspot.com).

Nikki Mbishi pia ameonesha wazi kutomkubali Bonta kama msanii hali inayoashiria kuwa ni ngumu kwa Bonta ama Weusi kwa ujumla kukaa kimya; “Ninaposema Bonta hayupo conscious namaanisha kuwa naheshimu anachofanya, ana ujumbe wa maana lakini uwasilishaji wa ujumbe wake kwa umma ndio tatizo. Kwa neno moja naweza kusema Bonta ni MC mbovu,na ninaposema hivyo namaanisha kuwa hajui kurap, anachofanya nikuongea na wakati mwingine anapata beat nzuri za kuongelea. Nadhani huu ni muda wa kuwaambia ukweli” (phatbeattz.blogspot.com)

Hata hivyo kama mwenzie One, Nikki Mbishi pia ameonesha wazi kung’ata na kupuliza kuhusiana na suala hili “if my mind is a belly then am bellyful I don't think if there is a space to put this cow meat a.k.a BEEF......”

Tayari mashabiki wa pande zote mbili wameanza kujihusisha moja kwa moja kwa kutoa mawazo yao katika kurasa za wasanii hao. “Tunachoshindwa kuelewa wabongo siku zote ni hiki.., Ukweli haui-justified kwa pesa, umaarufu na ujanja ujanja wa maneno. Muziki utabaki kuwa Muziki. Hip Hop itabaki kuwa Hip Hop. Kama "samaki Kwenye Hii Bahari" atazingua.., "tunamvua" tu kwani niaje...!? SUPPORT KWA Nikki Mbishi BabaMalcom NA WOTE WANAOSIMAMA FOR HIP HOP!!!”  


Wengine wameshindwa kuzuia chuki zao na kuandika maneno makali dhidi ya Weusi kuonesha namna wanavyoiunga mkono kambi ya akina Nikki Mbishi. “Watajichubua tu hao weusi. Watoto wazuri wanajiita weusi, hatutaki matozi. One, stereo na Nikki Mbishi wana big screen inayoönyesha u2po wa mabitch weusi. One wagonge ta**o, Nikki mbishi, wachinje huku wanakuchea, stereo watie vitasa watoto wanazingua”.

Vyombo vya habari husasan radio ambavyo siku zote vinaongoza kwa kukuza beef za aina hii vimechukua nafasi zao kwa kufanya mahojiano kupata ufafanuzi juu ya suala lenyewe hali inayolikuza zaidi.

 MLAB ambayo ni nyumbani kwa One, Nikki Mbishi na Stereo imeonesha kutofurahishwa na beef hiyo inayoendelea kukua kwa kasi. Meneja wa wasanii na Studio wa MLAB Patrick Gondwe amemuomba Nikki Mbishi kuachana na beef hiyo.  “ Kama kaka, nakuomba kuachana na suala hili Nikki! Kambi zote mbili ziache kuwagawa mashabiki…..Wapo kwa ajili yetu na hilo ni suala muhimu… Hatutakiwi kutawaliwa na vyombo vya habari.. Siku zote habari mbaya ni habari njema kwao….kutatokea mengi ya kuchanganya  lakini mwisho wa siku sisi tutapoteza mara mbili. Tukubali kukosa (lose) kwa kutokuandika vitu hasi kwenye mitandao ya kijamii na kuziba midomo yetu dhidi vyombo vya habari kuhusu suala hili. Nakuomba sana”

Uamuzi wa kukaa kimya kwa pande zinazohitirafiana unaweza kuwa na faida na hasara. Faida ni kuwa mashabiki wa pande zote mbili watapata fursa ya kuujua ukweli wa jambo lenyewe na kutafakari. Kwao Weusi na akina Nikki Mbishi wanaweza kutumia mahojiano na vyombo vya habari kuzuia kuwagawa mashabiki wao. Hasara ni pale ambapo pande hizi zitajikuta zikitumiwa na radio ama watu wenye lengo la kufanya biashara kupitia mgongo wao. Mfano halisi ni jinsi Darlive ilivyotumia beef ya Roma na Izzo kibiashara.

Kama beef hii ikiendelea kukua madhara yake yataenda mbali zaidi ya hapa ilipo. Beef hii inahusisha wasanii wanaowakilisha mikoa mikubwa yenye ushindani katika muziki wa hiphop, Arusha na Dar es Salaam. Kwa muda mrefu Arusha imekuwa ikitajwa kuwa ngome imara kwa hiphop nchini hivyo beef hii inatoa picha ya wazi ya ushindani kati ya Arusha na Dar es Salaam.

 Hatari ni pale mashabiki wa pande hizi mbili wakigawanyika katika misingi ya kimkoa. Ikiwa hivyo itakuwa ngumu kwa wasanii kama One, Nikki Mbishi na Stereo kwenda Arusha kufanya show wakihofia usalama wao. Historia ya mkoa wa Arusha inatueleza ni kwa kiasi gani watu wa huko walivyo na ushirikiano katika kupinga kitu wasichokipenda. Japo katika hiphop beef zina umuhimu wake, tuombee Mungu beef hii isije kufikia hatua ya watu kupigana wanted katika maskani zao bali kuwapa hasira za kiuandishi wote wanaohusika na mwisho wa siku kuwapa mashabiki muziki mzuri.


Fredrick Bundala aka Skywalker

Tone Radio

www.toneradiotz.com

No comments:

Post a Comment